.

Makala ya Michezo na Jackson mg.

Mwamuzi Kipunje, anachezesha mechi akiwa na Panga,shoka

Kwa ufupi
Ukimuuliza shabiki yeyote wa soka duniani, atakwambia kwa sasa kuna mwamuzi mmoja tu maarufu, Howard Webb.
Ukimuuliza shabiki yeyote wa soka duniani, atakwambia kwa sasa kuna mwamuzi mmoja tu maarufu, Howard Webb.
Sifa yake ni kuchezesha mechi ya fainali ya Kombe la Dunia kati ya Hispania na Uholanzi nchini Afrika Kusini mwaka 2010.
Pia hata mechi ngumu za Ligi Kuu England au Ligi ya Mabingwa Ulaya amekuwa akipangwa kuchezesha.
Sahau hilo la Webb. Tanzania kuna mtu mmoja anaitwa Kipunje.
Huyu jamaa anaishi sehemu moja inaitwa Mwananyamala B, Mtaa wa Ujiji, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Unaweza ukashangaa, lakini huyo Kipunje ndiyo mwamuzi ghali zaidi wa mechi za mchangani kwenye wilaya zote tatu za Dar es Salaam ambazo ni Temeke, Ilala na Kinondoni.
Ndiye mwamuzi pekee anayeweza kufanya kitu ambacho hata Webb au mwamuzi yeyote wa Fifa hawezi kuthubutu kukifanya.
Ndiye mwamuzi wa Dar es Salaam, ambaye ni maarufu zaidi katika mechi za mchangani na anayechezesha mechi yoyote iliyoshindikana kutokana na vurugu za mashabiki au wachezaji, haogopi chochote ndiyo maana thamani yake ipo juu tofauti na wengine.
Ukikutana naye ana kwa ana mtaani huwezi kuamini kwamba ndiye Kipunje anayeogopwa na wakorofi walioshindikana katika Wilaya ya Kinondoni.
Unajua kwa nini anaogopwa? Ni hivi, anachezesha mechi akiwa ametinga na silaha za jadi kiunoni ndani ya bukta yake. Silaha hizo ni panga refu upande wa kushoto na shoka dogo upande wa kulia.
Nani atamsogelea?
Anavyojiandaa anavaa jezi zake bukta, fulana, soksi na raba kisha anafunga kamba ya katani kiunoni halafu anachomeka panga kushoto kwake na shoka kulia.
Anachukua kadi zake ile ya njano anaweka mfuko wa kushoto kifuani kwenye fulana yake na ile nyekundu anaichomeka kulia ananyoosha viungo anaingia kazini.
Kivutio chake kikubwa ni silaha anazotinga na kujiamini ambako kumefanya timu zote korofi hata wahuni na mateja wanaoingia viwanjani kuogopa kumfanyia fujo kama wanavyofanyia waamuzi wengine.
Ndiye mwamuzi ghali zaidi. Kwa mechi moja hulipwa kuanzia Sh20,000 hadi Sh50,000 kulingana na ugumu na mazingira hatarishi kwenye mchezo husika.
Waamuzi wengine hulipwa kati ya Sh10,000 mpaka Sh12,000 kwenye mechi hizo. Kama ukiwa na kiasi hicho huwezi kuzungumza na Kipunje kwani ni ndogo mno kwake.
Mwamuzi huyo ambaye jina lake halisi ni Issa Salum Mchinjakuku.
‘Kipunje’, anasema Mchinjakuku ni jina la babu yake mzaa baba na ni mwenyeji wa Pwani.
Kwa nini anaitwa Kipunje?
“Niliitwa hilo jina kwa vile tangu nikiwa mdogo nilikuwa napenda sana ubwabwa wa kwenye hitma, huko pia pamenifanya kujulikana sana. Hata nikiwa na washikaji zangu tunashtuana ni wapi kwenye ubwabwa tuibuke. Pitapita zetu kwenye hiyo minuso zimenifanya nijulikane sana. Popote pale nakwenda ilimradi kuwe na ubwabwa.”
Chanzo cha kutumia silaha
Kipunje ambaye alizaliwa mwaka 1980 Mwananyamala jijini Dar es Salaam, anasema alianza kufanya hivyo mwaka 2005 baada ya kumshuhudia mwamuzi mwenzake aliyemtaja kwa jina la Wema akipigwa na mashabiki mpaka kuzirai.
“Tukio hilo lilitokea katika Uwanja wa CCM Mwinyijuma, Dar es Salaam ambako mashabiki wa timu ya Amstadam ya Tandale walimdunda Wema hadi akazimia, walifanya hivyo baada ya mwamuzi huyo kukubali bao la Mchangani FC ya Mwananyamala ambalo halikuwa na utata wowote.
“Niliumia sana kuona mwenzangu anapigwa hivyo bila ya kupata msaada wowote, tena ilikuwa karibu kabisa na kituo cha polisi, lakini alidundwa vibaya na hata Polisi walipoambiwa hawakutokea kumuokoa kwa sababu wanaujua mtiti wa wahuni wa Tandale,” anasema Kipunje ambaye anajitambulisha kuwa ni Mzaramo.
“Hali hiyo ndiyo iliyonifanya nipate akili ya kuingia uwanjani nikiwa na silaha, lengo likiwa ni kujilinda ili na mimi siku moja yasije kunikuta kama yaliyomkuta mwenzangu na kama unavyoona hakuna mhuni au mchezaji yeyote mkorofi anathubutu kunipiga iwe amekubaliana na matokeo au anapinga wanaishia kupiga kelele tu, lakini mimi nipo salama,” anasema Kipunje ambaye alianza kazi ya uamuzi wa soka mwaka 2000.
“Mwaka jana silaha hizi zilinisaidia na pengine kama nisingekuwa nazo siku hiyo ningekuwa sipo duniani sasa, ningekuwa marehemu, ilikuwa katika Uwanja wa CCM Mwinyijuma nilipokuwa nachezesha mechi ya nusu fainali kati ya Shideo na Baula.
“Mashabiki wa Shideo waliingia uwanjani kwa lengo la kunipiga kwa sababu tu nilikubali bao walilofunga Baula, jamaa walikuwa wamefura ile mbaya, niliwaacha wanisogelee kwani walikuwa hawajui kama nina vifaa vya kazi kiunoni.
“Walipofika na kuanza kunisukuma nilichomoa panga na wakashituka wakatoka nduki, hali iliyonipa ujasiri na mimi nikaanza kuwafukuza, lakini bahati mbaya panga liliniponyoka na kudondoka mbali kidogo na mimi.
“Mmoja kati ya mashabiki hao aliliwahi na kulichukua lakini kabla hawajakaa sawa nilichomoa shoka langu na kuanza kuwafuata kwa kasi ya ajabu, baada ya kuona hivyo jamaa alilitupa panga hilo na kutimua mbio kama vile wamemuona mtoa roho,” anasema mwamuzi huyo mwenye elimu ya msingi.
“Baada ya kuhakikisha wamefika mbali nilirudi uwanjani na kuendelea na kazi yangu na hakuna mtu yeyote aliyeleta tena chokochoko hadi mechi hiyo ilipomalizika. Kitendo hicho kilizidi kuniongezea umaarufu katika mitaa ya Mwananyamala, Kinondoni, Tandale na sehemu nyingine za Jiji la Dar es Salaam ambako mechi zote zinazohusisha timu zenye mashabiki wahuni, ninakodishwa nikachezeshe hakuna mtu yeyote anayeniletea upuuzi, nikitoa uamuzi hakuna anayebisha kama akipiga kelele ni huko huko nje ya uwanja.
“Mbali na mashabiki pia hata wachezaji na hata mateja ambao hukusanyika viwanjani nao wananifahamu sana na kuniogopa, tangu wajue nina silaha nikimwonyesha mchezaji kadi nyekundu hutoka nje kwa roho safi kabisa bila ya kunung’unika kwa sababu anajua akiniletea ujinga atakiona cha mtema kuni, silaha zimenifanya niwe mwamuzi wa bei mbaya kuliko wote Wilaya ya Kinondoni.”
Familia yake inamchukuliaje
Kipunje ni baba wa watoto watatu; Zainabu (5), Zulfa (2) na Nasra (1) na ni mume wa wake wawili anaoishi nao pamoja nyumbani kwake Mwananyamala.
Anasema kuwa familia yake haijui kama huchezesha soka akiwa na silaha hizo za jadi kwani anapotoka nyumbani kwenda kazini huzificha kwenye begi maalumu lenye jezi na vifaa vingine vya uamuzi.
“Wake zangu wote wananihesimu sana na hawajui chochote juu ya jambo hilo na hawajawahi kuniuliza, mara nyingi ninapokuwa naondoka nyumbani nahakikisha hizo silaha hawazioni, nafanya hivyo ili wasipatwe na wasiwasi waniogope, hiyo inaweza kusababisha mapenzi yetu yakayumba pia sipendi watoto wangu waone,”anasema mwamuzi huyo, ambaye ana kadi na jezi maalumu kwa mechi za mchangani na zile zinazoandaliwa na Chama cha Soka cha Kinondoni (Kifa).
Changamoto na malengo
Anasema viongozi wa Chama cha Soka Wilaya ya Kinondoni (Kifa) wamekuwa wakimuonya na kumtaka aachane na silaha hizo, lakini yeye amekuwa akigoma kwa vile ndiyo usalama wake anapokuwa uwanjani kwani mchangani hakuna usalama na ndiko anakopatia fedha nyingi za mkupuo.
Anasema pia staili yake ndiyo imepandisha thamani yake na endapo ataiacha ataporomoka na kupotea kwa vile atakuwa hana jipya.
“Siwezi kuacha silaha zangu iwe katika mechi za Kifa au zile za mchangani ambazo huandaliwa na watu wa kawaida, nitakuwa nahatarisha maisha yangu kwa sababu huko mashabiki hawafai hata kidogo wengi wanafuata fujo si mpira. Nimewaambia nitaachana na silaha nitakapofanikiwa kuwa mwamuzi wa Ligi Kuu Bara,” anasema Kipunje ambaye anadai ni mwamuzi wa Kifa baada ya kufanya vizuri kwenye mafunzo ya mwaka jana.
Lakini, Katibu Mkuu wa Chama cha Waamuzi Wilaya ya Kinondoni, Hussein Kalindo anasema: “Bado hajawa mwanachama wetu, ila alipata mafunzo na bado majibu yake ya mtihani hayajatoka.”
Malengo ya Kipunje
“Mungu akipenda mwezi Desemba nitahudhuria mafunzo ya TFF kujaribu bahati yangu ya kuchezesha Ligi Kuu. Nikifanikiwa kupata nafasi hiyo naamini kuwa heshima yangu itaongezeka pia nitaheshimu zaidi sheria 17 za soka na nitakuwa bora zaidi kama yule mwamuzi Hashim Abdallah aliyechezesha mechi ya Ligi Kuu ambayo Simba iliitandika Yanga mabao 5-0 au Pierluigi Collina yule Mitaliano ambaye amewahi kuwa mwamuzi bora wa Fifa,” anasema.
Kazi nyingine anayofanya
Ukiachana na uamuzi wa soka, Kipunje pia ni kondakta wa daladala inayofanya kazi ya kusafirisha abiria kutoka Makumbusho kwenda Kivukoni jijini Dar es Salaam.
“Kazi hii ya ukondakta naiheshimu sana kwani ndiyo inayonisaidia kwa kiasi kikubwa kuendesha maisha yangu ya kila siku na kuifanya familia yangu iwe na amani wakati wote japo kuna changamoto nyingi ambazo nakutana nazo,” anasema.

 

 

Tangaza hapa

Tangaza hapa

Burudani

Zinakuja..

Habari za Ulimwengu

zinakuja..
NukuuTz-2012. Powered by Blogger.
 
Support : Creating Website | Johny Template | Maskolis | Johny Portal | Johny Magazine | Johny News | Johny Demosite
Copyright © 2011. NANUKUU - All Rights Reserved
Template Modify by Creating Website Inspired Wordpress Hack
Proudly powered by Blogger